Waziri Mkuu Mizengo Pinda jana (Jumatatu, Novemba 18, 2013) aliongoza mamia ya waombolezaji katika mazishi ya aliyekuwa Mjumbe wa Tume na Mabadiliko ya Katiba na Kiongozi wa NCCR-Mageuzi Dkt. Sengomdo Mvungi yaliyofanyika katika kijiji cha Chanjale wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Pamoja na Waziri Mkuu aliyeongozana na mkewe, Mama Tunu, pia walikuwepo Mawaziri kadhaa kiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uratibu na Uhusiano) Steven Wassira aliyekabidhi ubani wa Rasi Jakaya Kikwete kwa familia.
Ibada ya mazishi iliendeshwa na Maaskofu watatu wakiongozwa Askofu Mkuu wa Jimbo la Kanisa Katoliki Arusha, Josephat Lebullu ambaye ni mwenyeji wa wilaya ya Mwanga. Wengine walikuwa Askofu wa Jimbo la Same Rogath Kimaryo na Askofu wa Jimbo la Geita Damian Dallu aliyesafiri kutoka Geita kuja kuungana na wenzake kumuaga Dkt. Mvungi.
Pamoja na Waziri Mkuu, mazishi hayo pia yalihudhuriwa na zaidi ya nusu ya wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakiongozwa na Mwenyekiti wake Jaji Joseph Warioba. Mawaziri wengine waliokuwepo ni Prof. Jumanne Maghembe (Maji) ambaye pia ni Mbunge wa Mwanga.
Wengine ni Dkt. Harrison Mwakyembe (Uchukuzi) na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Angellah-Jasmine Kairuki. Pia walikuwepo Wakuu wa mikoa ya Arusha (Mugessa Mwalongo) na Kilimanjaro Leonidas Gama.
Kwa upande wa NCCR-Mageuzi, uongozi wote wa juu wa Chama hicho ulikuwepo ukiongozwa na Mwenyekiti wake James Mbatia ambaye aliiomba Serikali kuimarisha ulinzi na usalama wa wananchi na mali zao.
Pamoja nao, kulikuwa na wawakilishi kadhaa wa taasisi mbalimbali ambazo marehemu Dkt. Mvungi alifanya nazo kazi wakati wa uhai wake. Taasisi hizi ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es salaam ambacho kiliwakilishwa na Mkuu wa Shule Kuu ya Sheria Prof. Bonaventure Rutinwa, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kilichowakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Hellen Kijo-Bisimba; Chuo Kikuu cha Bagamoyo (UB) na Chama cha Wanasheria Tanzania Bara (TLS) kilichowakilishwa na Wakili Eric Ngimaryo na mawakili wengine kadhaa kutoka mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.
Dkt. Mvungi alifariki nchini Afrika Kusini alikokuwa amepelekwa kwa ajili ya uchunguzi na matibabu Zaidi akitokea Kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI) alikokuwa amelazwa baada ya kuvamiwa nyumbani kwake Kibamba, wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na watu waliomjeruhi vibaya kichwani usiku wa kuamkia siku ya Jumapili, Novemba 3, 2013.