WABUNIFU mbali mbali kupamba miaka 10 ya onyesho la mavazi lijulikanalo kama ‘Lady in Red Super brand, 10th Anniversary’ linalotarajiwa kufanyika Februari 14, ambapo pia litatumbuizwa na burudani kutoka kwa Babloom Trio bendi na Wanne Star, kwenye Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Fabak Fashions inayoandaa onyesho hilo, Asia Idarous Khamsin, alisema tayari maandalizi ya onyesho hilo yameshakamilika na tayari wabunifu mbalimbali wameanza mchakato wa kuandaa mavazi yao watakayoonyesha siku hiyo.
Asia Idarous alipongeza wadau mbali mbali kwa kuliunga mkono onyesho hilo la ‘Lady in red’ hadi kufikisha miaka 10, tokea kuanzishwa kwake, na kutamba kuwa la kipekee kwa mwaka huu.
“Februari 14, mwaka huu ndiyo siku pekee kwa wadau wa mitindo na urembo ambapo watashuhudia wabunifu mbalimbali siku hiyo wakipamba jukwaa, wakiwemo wakongwe na wale wanaochipukia” alisema Asia Idarous.
Na kuongeza kuwa, kwa mwaka huu wametoa fursa kwa wabunifu wanaochipukia kuonyesha mitindo yao sambamba na wakongwe ili kuleta changamoto kwen ye tasnia hiyo ya ubunifu na mitindo hapa nchini.
Aidha, katika onyesho hilo ambalo litafanyika siku hiyo ya Februari 14, ambayo pia itakuwa ni siku ya Wapendanao ‘Valentine’s Day’ , kiingilio kitakuwa sh 30,000 kwa viti vya kawaida huku viti maalum ikiwa sh 50,000, ambapo pia kutakuwa na burudani kutoka bendi ya Babloom Trio na Mwanamuziki mahiri wa nyimbo na ngoma za asili, Wanne Star.